Alex Augustine mkazi wa kitongoji cha Kashai mjini Sumbawanga amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na kosa la kulawiti mtoto wa kiumwe mwenye umri wa miaka tisa (9).
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya
Sumbawanga, Uutor Bigambo, baada ya kusikiliza pande zote na kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasipokuacha shaka.
Alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Novemba 2020 hadi Novemba 27, 2021, katika kitongoji cha Kashai, mjini humo.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa ambaye alikuwa ni dereva bodaboda alikuwa na utaratibu wa kumpokea mtoto kutoka katika moja ya basi la shule na kumpeleka nyumbani.
Alisema mara kadhaa baada ya mshtakiwa kumpokea mtoto huyo alikuwa akimpeleka katika moja ya nyumba ambayo bado haijaisha (pagale) na kuanza kumwingilia kinyume na maumbile huku akimtishia asiseme kwa wazazi wake kwa madai akithubutu kufanya hivyo atamuua.
Hakimu huyo alisema wakati mshtakiwa akiendelea kufanya kosa hilo, ilibainika kwamba mtoto akilalamika maumivu makali ndipo walipomuhoji na kueleza kile anachofanyiwa na kijana huyo.
Wazazi wa mtoto huyo walimchukua mtoto na kutoa taarifa polisi na kwenda kupimwa hospitali, ambako ilibainika analawitiwa na sehemu yake ya haja kubwa imeanza kuharibika.
Mshtakiwa Augustine alikimbia kuelekea mkoani Katavi alikokaa kwa miezi kadhaa, lakini polisi walimkamata.
Hakimu Bigambo alisema kutokana na maelezo ya pande zote mbili inathibitisha alitenda kosa hilo na utetezi wake (Agustino) hauna mashiko Mahakama inamhukumu kifungo cha maisha jela.
0 Maoni